MKATABA WA HUDUMA KWA WATEJA
Zifuatazo ni Haki na Wajibu wa Mteja (Mgonjwa):
HAKI ZA MTEJA.
1. Kupata Huduma.
Unayo haki ya kupata huduma mbalimbali za kitabibu zinazotolewa na Hospitali, kulingana na mahitaji yako ya kiafya. Pia kwa mujibu wa ushauri wa Daktari.
2. Kupata Taarifa.
Unayo haki ya kupewa taarifa kamilifu kuhusu afya yako, matibabu stahiki na matokeo yake. Utapewa muda wa kutosha kuuliza maswali, kupata taarifa za ziada, kuongea na ndugu na marafiki kabla hujafanya uamuzi wa mwisho.
3. Haki ya Kujieleza.
Una haki ya kujiridhisha, kutoa maoni au kalalamikia (kwa njia ya staha) kuhusu huduma ya afya uliyopewa na kupewa mrejesho.
4. Haki ya Kupata Maoni ya Pili.
Unayo haki ya kupata maoni ya kitabibu kutoka kwa mtaalam mwingine wa afya, ndani ya hospitali au kwingineko.
5. Haki ya Heshima, Utu na Usiri.
Hospitali itakupa huduma ya kitabibu katika mazingira yanayozingatia faragha yako. Utahudumiwa kwa kuzingatia utu wako bila ubaguzi wa aina yoyote.
6. Haki ya Huduma ya Viwango.
Una haki ya kupata matibabu kulingana na hali yako kiafya na kulingana na viwango na taratibu zinazokubalika.
7. Haki ya Kuwa na Mwenza.
Unayo haki ya kuambatana na mwanafamilia, rafiki au mtu mwingine unayependa kuwa nae wakati wa kuonana na Daktari.
8. Huduma Itatolewa kwa Kuzingatia Mila na Imani ya Mtu.
Unayo haki ya kuhudumiwa kulingana na mila na imani yako. Watoa huduma hospitalini watafanya kila liwezekanalo kuendana na mahitaji na matarajio ya mila na imani yako.
9. Haki ya Kukataa au Kukubali Matibabu.
Unayo haki ya kupata maelezo ya kina kuhusu aina ya tiba inayopendekezwa kabla ya kuitumia na mbadala wake na una haki ya kuikubali au kuikataa.
10. Kupata Taarifa za Kitabibu na Usiri Kuhusu Taarifa Binafsi.
Unaweza kutaka kuona taarifa za kumbukumbu ya ugonjwa na matibabu yako wakati wowote uwapo hospitali, au baada ya kuruhusiwa, au baada ya kupata matibabu.
Kila atakayehusika katika kukuhudumia na/au kukutibu, anawajibika kiweledi na kisheria kutunza siri za taarifa za ugonjwa wako.
Taarifa kuhusu ugonjwa na matibabu haziwezi kutolewa kwa mtu yeyote ambaye hausiki na matibabu, isipokuwa kwa idhini ya mgonjwa husika au kwa amri ya Mahakama.
WAJIBU WA MTEJA.
1. Wajibu wa Kutoa Taarifa Sahihi.
Toa ushirikiano kwa matabibu wote wanaokuhudumia kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu hali yako na uwe na mwenendo ambao hautawachukiza au kuwakwaza kwa namna ambayo itaathiri matibabu, kupona kwako au muda wako wa kukaa hospitalini.
2. Wajibu wa Kuheshimu Watoa Huduma.
Unawajibika kuenenda kwa namna ambayo haitawaudhi au kuwavunjia heshima watoa huduma hospitalini wa ngazi zote.
3. Wajibu wa Kutunza Vifaa na Vitendea Kazi.
Tumia vifaa na vitendea kazi vya hospitali kwa uangalifu na bila kuleta usumbufu kwa watu wengine.
4. Wajibu wa Kutunza na Kuweka Mazingira Safi.
Unatakiwa kutunza usafi wa mazingira na vifaa vya hospitali, pia kuepuka kueneza magonjwa.
5. Wajibu wa Kuheshimu Watu Wengine
Unatakiwa kuonesha heshima, uvumilivu na kuwajali wagonjwa wengine. Ndugu na watu wote bila kujali matendo yao au hadhi yao.
6. Wajibu wa Kuheshimu Kanuni na Taratibu za Hospitali.
Wagonjwa na ndugu zao wanatakiwa kuzingatia kanuni na taratibu za hospitali, ili kuwezesha utoaji huduma usio na vikwazo.