Sifa muhimu za ugonjwa wa akili ni kuvurugukiwa kwa hisia, mawazo au tabia za watu. Jambo ambalo ni nje ya utaratibu uliozoeleka wa imani zao za kitamaduni na nafsi zao. Na upelekea kutokea kwa athari hasi katika maisha yao na familia zao.
Magonjwa ya akili yaliyo kali, yana kawaida ya kuwa sugu kutokea kwa vipindi na sio mfululizo. Na huwa na athari za muda mrefu kuhusu kupungua kwa uwezo wa kutenda mambo.
Dalili za Magonjwa ya Akili ni pamoja na:
- Mvurugiko wa namna watu wanavyofikiri- kufasiri mambo kinyume na namna yalivyo, na kwa mtazamo uliobadilika (maono).
- Mvurugiko wa namna watu wanavyotambua vitu kwa macho, masikio, kunusa, kuonja na kugusa- wanaona mambo ambayo watu wengine hawayaoni. Kwa mfano; kuona au kusikia mambo yasiyoweza kuonekana au kusikiwa na wengine.
- Kuvurugukiwa kwa hisia- mara nyingi kunaambatana na kupoteza uwezo wa kufikiri. Kama vile kuwa na hofu kupita kiasi, kuwa na mawazo hasi na kudhihirisha msongo wa kisaikolojia kwa dalili zinazoonekana kwenye mwili.
- Watu wenye msongo au mfadhaiko wanaweza kujaribu kukabiliana na dalili walizonazo kwa kutumia mihadarati au pombe.
Magonjwa yanayotokana na matumizi ya mihadarati/pombe yameenea sana katika jamii zetu. Na kwa ujumla yana athari sana kwenye jamii katika uzalishaji, afya na usalama. Pombe inatumika vibaya zaidi katika jamii nyingi za Kitanzania ikifuatiwa na tumbaku na bangi.
Vitu vingine ni pamoja na uvutaji wa vitu vyenye kulevya (petroli, mafuta ya taa, gundi, na kadhalika), miraa na heroini.
Madhara ya kutumia Mihadarati au Pombe vibaya.
- Visababishi vya magonjwa mbalimbali.
* Magonjwa yasiyo ya yakuambukiza kama vile kisukari na magonjwa ya moyo (pombe).
* Magonjwa sugu ya mapafu na saratani za matumbo (tumbaku).
- Uharibifu wa viungo vya mwili- pombe inaweza kuharibu ubongo, moyo, ini, na kadhalika.
- Utapiamlo kutokana na lishe duni.
- Kupungua kwa uwezo wa uzalishaji kwenye jamii.
- Kuongezeka kwa migogoro kwenye familia na katika ngazi za jamii.
- Kuongezeka kwa tabia za kiharifu kwenye jamii, kutokana na:
* Tabia zinazohusiana na kuathiriwa na dutu hizi.
* Umiliki wa dutu haramu.
* Hatua zilizochukulikwa kinyume na sheria katika upatikanaji wa dutu hizo pale wahusika wanapokuwa tegemezi.
- Utegemezi wa kisaikolojia- wale wanaoathirika wanadhani kuwa hawawezi kutimiza vizuri majukumu yao ya kijamii, mpaka kwanza watumie dutu hizo.
- Utegemezi wa kimwili- fiziolojia ya mwili inabadilika na kuzoea uwepo wa dutu hizo kwenye mwili, kiasi kwamba pale mtu anapopunguza matumizi yake, dalili bayana za mwili huweza kutokea kuashiria upungufu fulani (hususan kwa pombe na heroini).
MUHIMU: Magonjwa ya akili yanatibika, na mengi yanaweza kudhibitiwa katika ngazi ya zahanati. Kwa ushirikiano wa ziada kutoka kwa mtumishi wa afya ya jamii na wanajamii wenyewe kwa ujumla.